RC Chacha Aongoza waombolezaji mazishi ya Mhe. Paschal Kigalu
Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha, ameongoza madiwani, watumishi wa Halmashauri ya Mji wa Nzega pamoja na wananchi kwa ujumla katika mazishi ya mwili wa Mhe. Paschal Kigalu.
Mhe. Kigalu, aliyekuwa Diwani wa Kata ya Itilo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Nzega, alifariki tarehe 17 Februari 2026 baada ya gari alilokuwa akiendesha kuhusika katika ajali iliyotokea eneo la Kitangili, karibu na stendi ya mabasi ya Nzega.
Mazishi hayo pia yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali na vyama vya siasa, walioungana na mamia ya waombolezaji wakiwemo viongozi wa dini na wananchi wa Nzega, kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa marehemu.
Akizungumza katika mazishi hayo, Mkuu wa Mkoa Tabora alitoa pole kwa familia, ndugu na wananchi wa Nzega kwa msiba huo mzito.
“Tuwe wavumilivu katika kipindi hiki kigumu na tufanye juhudi kuyaenzi mema yote aliyoyafanya marehemu katika kuwatumikia wananchi wa Kata ya Itilo na Halmashauri ya Nzega Mji kwa ujumla,” alisema.
Aliongeza kuwa mchango wa marehemu katika maendeleo ya eneo hilo utaendelea kukumbukwa, huku akihimiza umoja na mshikamano ili kuendeleza yale mema aliyoacha.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Nzega, Bwana Shomary Mndolwa, akishirikiana na wakuu wa idara na watumishi wa umma, alisema wameendelea kuwa pamoja na familia ya marehemu katika kipindi chote cha msiba hadi mazishi yalipokamilika na mwili wa marehemu kuzikwa kwenye makazi yake ya milele.
“Hili ni pigo kubwa kwetu kama Halmashauri, na tunaomba Mwenyezi Mungu amlaze mahali pema peponi,” alisema Mkurugenzi huyo.
Mbunge wa jimbo la Nzega mjini Mhe. Hussein Bashe alihudhuria msiba huo na kumweleza Marehemu kama mpenda maendeleo na rafiki yake wa kisiasa wa muda mrefu.
Baadhi ya nyadhifa alizowahi kushika marehemu enzi za uhai wake ni pamoja na uwenyekiti wa CCM kata ya Itilo. Pia amekuwa Diwani wa kata hiyo tangu mwaka 2015 had umauti ulipomkuta.
Tarehe 5, Disemba 2025, Marehemu alichaguliwa kwa kishindo kuwa mwenyekiti wa halmashauri ya Mji Nzega, nafasi aliyehudumu kwa miezi miwili na siku 12 hadi hadi tarehe 17, Februari mwaka huu
NZEGA TOWN COUNCIL (HALMASHAURI YA MJI NZEGA)
Sanduku la Barua: S.L.P 256 NZEGA-TABORA
Simu ya Mezani: +255677003373
Simu ya Mkononi: +255677003373
Barua Pepe: td@nzegatc.go.tz
Haki miliki zote zimehifadhiwa na nzegatc 2017