JAMES KAMALA, Afisa Habari, Nzega Mji
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Isdor Mpango, amewataka wakazi wa Mji wa Nzega kujiandaa kikamilifu kushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi Novemba 2024. Dkt. Mpango amesema kuwa wananchi wajiandae kwa kujiandikisha kwenye Daftari la Wapiga Kura ili watambulike rasmi na waweze kushiriki katika kuchagua viongozi sahihi watakaowaletea maendeleo wanayoyataka.
Dkt. Mpango alitoa wito huo siku ya Jumanne, tarehe 8 Oktoba 2024, alipokuwa akizungumza na wananchi eneo la Soko la Machinga lililopo katikati ya Mji wa Nzega. Alisimama eneo hilo kuwasalimu wananchi wakati akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Tabora, akikagua miradi mbalimbali ya maendeleo na kuzungumza na wananchi.
"Niwatake wanawake hasa wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wajitokeze kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali za uongozi wa serikali za mitaa, na wapewe nafasi za kugombea ndani ya chama chetu," alisema, na kuongeza kuwa chama hicho kimekuwa kikitoa viongozi wanawake shupavu kama ilivyo kwa Rais wa sasa, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mhe. Dkt. Mpango pia amewasihi wananchi wa Nzega, pamoja na kujitokeza kujiandikisha na kupiga kura, wajilinde dhidi ya vurugu zozote ambazo zinaweza kuathiri zoezi la uchaguzi. Alisisitiza kuwa serikali iko macho na haitasita kuchukua hatua kali dhidi ya wale watakaojaribu kuhatarisha amani.
Kuhusu ujenzi wa Soko Jipya la Machinga unaotarajiwa kuanza hivi karibuni, Mhe. Makamu wa Rais aliagiza mamlaka za Wilaya ya Nzega kuhakikisha wafanyabiashara wadogo wanapewa kipaumbele kwenye ugawaji wa vizimba baada ya ujenzi kukamilika.
Naye Mbunge wa Jimbo la Nzega Mjini, Mhe. Hussein Bashe, alimweleza Mhe. Makamu wa Rais kuwa jimbo hilo linafanya vyema kwenye sekta ya elimu na kwamba wananchi wanapata maji safi na salama kutoka Ziwa Viktoria. Mhe. Bashe aliongeza kuwa miradi ya kuunganisha umeme inaendelea vizuri, na asilimia kubwa ya wakazi wa Nzega wameunganishwa na umeme majumbani mwao.
NZEGA TOWN COUNCIL (HALMASHAURI YA MJI NZEGA)
Sanduku la Barua: S.L.P 256 NZEGA-TABORA
Simu ya Mezani: +255677003373
Simu ya Mkononi: +255677003373
Barua Pepe: td@nzegatc.go.tz
Haki miliki zote zimehifadhiwa na nzegatc 2017