Na James Kamala, Afisa Habari
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tabora, Bwana Said Juma Nkumba, amesema miradi mikubwa ya maendeleo inayotekelezwa kwa ufanisi mkubwa katika Halmashauri ya Mji wa Nzega imefanikishwa na watumishi wa umma wenye moyo wa kujitolea, bidii, na kujituma.
Bwana Nkumba alitoa kauli hiyo katika ziara yake kwenye ofisi za Halmashauri ya Mji wa Nzega na kufanya kikao na watumishi wa kada mbalimbali katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo iliyoko eneo la Ipazi, Nzega Mjini.
“Niwapongeze sana watumishi wa umma kwenye Halmashauri hii kwa juhudi na bidii zenu za kufanya kazi usiku na mchana bila kuchoka, na kuhakikisha miradi ya maendeleo ya wananchi inatekelezwa kwa ufanisi mkubwa sana. Nampongeza pia Mkurugenzi wa Halmashauri hii, Bwana Shomary Mndolwa, kwa kuwa chachu ya mafanikio hayo,” alisema.
Aliongeza kuwa Serikali imekuwa ikitenga na kuleta fedha kwa ajili ya miradi mbalimbali, mbali na elimu, afya, kilimo, miundombinu, maji, na kadhalika, na yote imetekelezwa vyema, ikiwapatia wakazi wa Mji wa Nzega ahueni ya maisha yao ya kila siku.
Bwana Nkumba alisisitiza kuwa watumishi wa umma wamekuwa mstari wa mbele kutumia taaluma zao na hata kufanyakazi usiku ili miradi ya maendeleo ikamilike kwa wakati. “CCM Mkoa wa Tabora imekuja hapa kusema asanteni sana watumishi wa umma kwa moyo wenu huu wa kufanya kazi kwa bidii na kwa utaalamu wa hali ya juu sana.”
Mwenyekiti huyo wa CCM Mkoa wa Tabora alieleza shukrani zake kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye pia ni Mwenyekiti wa chama hicho taifa, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuajiri watumishi wengi wa kada mbalimbali ambao wamekuwa nguvu kubwa ya kusukuma gurudumu la maendeleo.
Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya watumishi wenzake, Mkuu wa Idara ya Rasilimali Watu ya Halmashauri ya Mji wa Nzega, Bi. Leah Kibaki, alisema CCM imekuwa karibu sana na kutoa ushirikiano unaohitajika kuhakikisha kila jambo linaenda kama inavyotakiwa.
“CCM Wilayani Nzega imekuwa ikitulea na inaendelea kutulea vizuri sana na hii inatuwezesha kutekeleza ilani ya uchaguzi kwa wepesi zaidi,” alisema.
NZEGA TOWN COUNCIL (HALMASHAURI YA MJI NZEGA)
Sanduku la Barua: S.L.P 256 NZEGA-TABORA
Simu ya Mezani: +255677003373
Simu ya Mkononi: +255677003373
Barua Pepe: td@nzegatc.go.tz
Haki miliki zote zimehifadhiwa na nzegatc 2017