*WANAFUNZI 1,126 WA SEKONDARI NZEGA MJINI KUFANYA MTIHANI WA KIDATO CHA NNE MWAKA 2025*
Wanafunzi 1,126 kutoka shule kumi na tano (15) za sekondari zinazomilikiwa na serikali kupitia Halmashauri ya Mji wa Nzega wanatarajiwa kufanya Mtihani wa Taifa wa kumaliza Kidato cha Nne mwaka 2025.
Mtihani huo unaoendeshwa na Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA) unatarajiwa kuanza mapema mwezi ujao na utafanyika nchi nzima kwa wakati mmoja.
Afisa Elimu wa Halmashauri ya Mji wa Nzega, Mwl. Leah Katamba, amesema kuwa tayari mikakati imewekwa ili kuhakikisha ufaulu wa asilimia tisini na nane (98%) kwa watahiniwa wa Halmashauri hiyo. Aliongeza kuwa lengo ni kuwa na ufaulu wa Daraja la Kwanza hadi la Nne, huku ufaulu wa Daraja la Kwanza hadi la Tatu ukitarajiwa kufikia asilimia sitini na tano (65%).
Mwl. Leah alitoa ufafanuzi huo katika kikao kilichowakutanisha Maafisa Elimu Kata, Wakuu wa Shule na Walimu wa masomo ya madarasa ya mtihani kwa lengo la kujadili kwa pamoja mikakati ya ushindi. Alibainisha kuwa ili kufanikisha malengo hayo, walimu wa masomo husika wanatakiwa kuongeza juhudi katika ufundishaji na kuhakikisha kuwa mada zote za mtaala zinamalizika kwa wakati.
Mikakati mingine iliyowekwa ili kuongeza ufaulu ni pamoja na kuwapa wanafunzi mazoezi na mitihani ya majaribio mara kwa mara, kudhibiti utoro wa wanafunzi na kuhamasisha utaratibu wa kujisomea nyumbani na shuleni kwa wakati wa kutosha.
Akifungua kikao hicho, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Nzega, ambaye pia alikuwa mgeni rasmi, Bw. Shomary S. Mndolwa, aliwaasa walimu kuwa waangalifu na kuepuka vitendo vya udanganyifu wakati wa mitihani. Alisema kuwa serikali haitavumilia vitendo vya wizi wa mitihani na hatua kali zitachukuliwa kwa yeyote atakayebainika kujihusisha na vitendo hivyo.
“Kile tunachokitaka ni ufaulu, na tunatarajia kazi yenu njema itawezesha hilo. Lakini vitendo vyovyote vya wizi wa mitihani na udanganyifu havitavumiliwa kabisa,” alisema Bw. Mndolwa.
Kuhusu motisha kwa walimu, Bw. Mndolwa aliahidi zawadi nono kwa walimu wa shule zitakazofanikisha ufaulu mkubwa, hasa kwa shule zitakazotoa watahiniwa waliofaulu kuanzia Daraja la Kwanza hadi la Tatu bila kuwa na mwanafunzi wa Daraja la Sifuri. Alisema zawadi hizo ni pamoja na ziara ya kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo ndani ya nchi.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA), mtihani wa kumaliza Kidato cha Nne mwaka 2025 unatarajiwa kuanza rasmi tarehe 10 Novemba 2025, na utahusisha wanafunzi kutoka shule za serikali na binafsi kote nchini.
NZEGA TOWN COUNCIL (HALMASHAURI YA MJI NZEGA)
Sanduku la Barua: S.L.P 256 NZEGA-TABORA
Simu ya Mezani: +255677003373
Simu ya Mkononi: +255677003373
Barua Pepe: td@nzegatc.go.tz
Haki miliki zote zimehifadhiwa na nzegatc 2017