Na James Kamala, Afisa Habari, Halmashauri ya Mji Nzega.
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deus Clement Sangu amewataka watumishi wa umma kuwa wabunifu na kufanya kazi kwa bidii katika kuwahudumia wananchi ili kuleta tija kwa maendeleo ya taifa. Aidha, Mhe. Naibu Waziri huyo amewataka waajiri wote katika utumishi wa umma kuhakikisha wanafanya kazi kwa karibu na watumishi ili kuepusha migogoro isiyo na tija kwenye utumishi wa umma.
Aliyasema hayo siku ya Ijumaa ya tarehe 20/09/2024 aliposikiliza na kutatua kero mbalimbali zinazowakabili watumishi wa Halmashauri ya Mji wa Nzega ikiwa ni sehemu ya ziara yake mkoani Tabora. “Watumishi wa umma mnapaswa kufanya kazi kwa kuzingatia nidhamu, ubunifu, kuboresha na kutathmini utendaji wenu ili wananchi waweze kupata matokeo chanya kwenye huduma wanazopatiwa,” alisema Mhe. Sangu.
Aliongeza kuwa Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imekuwa ikitenga na kutuma fedha za miradi ya maendeleo kwenye sekta mbalimbali kama vile afya, elimu na miundombinu, na hivyo ni wakati sasa wa watumishi wa umma kuhakikisha wanakuwa na utendaji unaoendana na kasi hiyo.
Kwa upande wa upungufu wa watumishi katika Halmashauri ya Mji wa Nzega na Mkoa wa Tabora kwa ujumla, Mhe. Sangu alisema tatizo hilo tayari limepatiwa ufumbuzi kwani mchakato wa kuajiri watumishi wa kuziba upungufu huo tayari umeanza. “Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ametoa vibali vya ajira mpya zaidi ya elfu arobaini na saba (47,000), na tayari Mkoa wa Tabora unatarajia kupata watumishi wapya zaidi ya elfu nne (4,000), tukianza na kada za afya,” alieleza Mhe. Sangu.
Kuhusu upandishaji wa vyeo kwa watumishi wa umma, Naibu Waziri huyo alisema kuwa serikali imekwisha tenga fedha za kutosha kwa ajili ya mchakato huo, ikiwemo pia fedha za kulipa madeni mbalimbali kama vile malimbikizo ya mishahara ya watumishi.
Wakati huohuo, Mhe. Sangu aliwaasa waajiri kuhakikisha wanatoa mafunzo ya awali kazini kwa watumishi wapya ili waweze kujua wajibu wao na haki zao, na hivyo kuepusha migogoro kazini na mashauri ya kinidhamu katika maeneo ya kazi.
“Wajulisheni na kuwaelekeza mazingira ya kazi, kanuni, na sheria za utumishi wa umma ili waweze kufanya kazi kwa uhuru na amani yenye tija kwa utendaji uliotukuka,” alisisitiza Mhe. Sangu.
Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Nzega, Mhe. Naitapwaki Tukai, Kaimu Katibu Tawala wa Wilaya hiyo Ricardo Katambi Komanya, pamoja na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Nzega, Bi. Leah Kibaki, na watumishi kutoka Idara na Vitengo mbalimbali katika Halmashauri hiyo.
Mwisho.
NZEGA TOWN COUNCIL (HALMASHAURI YA MJI NZEGA)
Sanduku la Barua: S.L.P 256 NZEGA-TABORA
Simu ya Mezani: +255677003373
Simu ya Mkononi: +255677003373
Barua Pepe: td@nzegatc.go.tz
Haki miliki zote zimehifadhiwa na nzegatc 2017