HALMASHAURI ya Mji Nzega imefanikiwa kuhamisha mabasi yote ya abiria ambayo yalikuwa yakitumia Stendi ya zamani katika upakiaji na ushushaji wa abiria kutoka mjini kwenda katika eneo la Sagara ambalo lina ukubwa wa ekari 10 kwa ajili kuondoa msongamano katikati ya Mji .
Hatua hiyo imefikiwa baada ya Halmashauri kufanikiwa kuweka miundo mbinu yenye thamani ya milioni 277.7 ambayo imesaidia katika hatua za awali za ufunguzi wa Stendi mpya ambayo itatoa huduma kwa magari ya abiria yanayopitia Mkoani Tabora na yale kutoka Mkoani hap.
Kauli hiyo ilitolewa tarehe 02.08.2018 na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Nzega Ndugu Philemon Magesa wakati wa sherehe fupi za uzinduzi wa Stendi hiyo iliyopo kando kando ya barabara kuu ya kwenda Shinyanga na Singida na maeneo mengine .
Alisema kwa kuwa Nzega iko kwenye njia panda, eneo la Stendi ya mabasi ya zamani lilikuwa dogo na kulifanya kushindwa kuhimili wingi wa mabasi yaliyokuwa yakitoka nje ya Nchi na yale ya mikoa mbalimbali ambayo yalikuwa yakipitia Nzega na kusababisha msongamano na karaha kwa wasafiri na watumiaji wengine wa barabara.
Mkurugenzi alisema baada ya kuona Halmashauri haiwezi kukamilisha kazi zote kwa wakati mmoja waliamua kutumia fedha hizo kidogo kuanza na hatua za awali za kujenga jengo la kupumzikia abiria, Kituo Kiodogo cha Polisi, vibanda sita(6) vya kukatia tiketi, vyoo na ofisi, vibanda vya askari , Mamlaka ya Usafirishaji Tanzania(SUMATRA) na kulipa fidia wananchi waliokuwa katika eneo ilipojengwa Stendi.
Mkurugenzi alisema, kazi nyingine ilikuwa ni kujenga uzio wa nyaya kuzunguka eneo la stendi,vibanda vya askari wa usalama barabarani, wakusanyaji mapato ya Halmashauri, kuweka taa za mwanga wa jua katika Ofisi kwa ajili ya kuimarisha usalama nyakati za usiku .
Alisema gharama halisi ya kujenga Stendi hiyo hadi kukamilika kwa kiwango cha juu kulingana na michoro ya ubunifu zinahitajika bilioni 7.7 ambapo kwa kutumia mapato ya Halmashauri ya ndani itachukua miaka 10 ili kukamilisha ujenzi wake.
Mkurugenzi alisema kutokana na kuhitajika fedha nyingi kukamilisha ujenzi wote limefanyika uamuzi wa kuandika andiko maalumu kwa ajili ya mradi huo na kuuwasilisha Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kupitia Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ambapo limeshawalishwa Wizara ya Fedha na Mipango ili kuweza kupatiwa fedha za kukamilisha ujenzi wa mradi huo mapema.
Alisema mara baada ya kukamilika kwa ujenzi wake kutaweza kusaidia Halmashauri kuongeza uwezo wa kukusanya mapato yake na ndani na kuiwezesha kuelekea katika kujitegemea.
Katika hatua nyingine Mkurugenzi alisema wako katika hatua ya mwisho ya kupata eneo lenye ukubwa wa ekari 15 kwa ajili ya kuweka maegesho ya magari ya mizigo ambalo nalo litasaidia kuingizia Halmashauri mapato yake ya ndani.
Kwa upande wa Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri alilitaka Jeshi la Polisi Wilaya ya Nzega kushirikiana na Halmashauri kuhakikisha wanaimarisha ulinzi katika eneo hilo saa zote kwa kuwa ni jipya na liko mbali na makazi ya watu. Upo uwezekano wa watu ambao sio wema wakatumia nafasi hiyo kutenda uovu wa aina mbalimbali ikiwemo kuwapora abiria.
Alisema uhalifu wa aina yoyote ukitokea unaweza kuwakatisha tamaa wasafiri na wawekezaji ambao wangependa kutumia Stendi hiyo jambo ambalo linaweza kusababisha mapato ya Halmashauri kupungua kutokana na wasafiri kuwa na hofu. .
Aidha Mkuu wa Mkoa alioutaka uongozi wa Halmashauri kuhakikisha huduma mbalimbali kama vile vyoo na kuweka vifaa vya taka zinakuwepo ili kuepuka magonjwa ya mlipuko wakati wa masika.
Naye abiria kutoka Yelayela wilayani Urambo kwenda Dar es salaam Mashaka Maganga aliipongeza Halmashauri kwa uamuzi wake wa kuihamisha Stendi kutoka mjini kuiweka eneo la Sagara kwani limesaidia kuondoa msongano sio tu magari hata abiria walikuwa wanapata shida kutokana na kuwa wengi katika eneo dogo.
NZEGA TOWN COUNCIL (HALMASHAURI YA MJI NZEGA)
Sanduku la Barua: S.L.P 256 NZEGA-TABORA
Simu ya Mezani: +255677003373
Simu ya Mkononi: +255677003373
Barua Pepe: td@nzegatc.go.tz
Haki miliki zote zimehifadhiwa na nzegatc 2017