TASAF ILIVYOKWAMUA UCHUMI WA KAYA MASKINI HALMASHAURI YA MJI NZEGA
Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) unaotekeleza Mpango wa Kunusuru kaya Maskini umekua chachu ya ukuaji wa uchumi kwa walengwa wa Mpango huu ambapo kwa Halmashauri ya Mji wa Nzega imekwisha pokea kiasi cha Tsh 716,782,351.00 kwa kipindi cha Julai 2020 hadi Julai 2022 ambacho kimenufaisha kaya 1,733.
Mratibu wa TASAF Halmashauri ya Mji wa Nzega Bw.Denis Kazinja Anasema,”TASAF imewezesha walengwa kujikita katika shughuli za uzalishaji mali kama vile kilimo,ufugaji na biashara ndogo ndogo na mahitaji mengine ya kijamii hali inayobadilisha uchumi wao kwa kuanza kujiingizia vipato ambavyo vinawawezesha kukidhi mahitaji yao ya kila siku”.
Mmoja kati ya wanufaika hao, Bi. Consolata Michael(47) mama wa watoto wawili na mjukuu mmoja anayeishi na mume wake mtaa wa Utemini kata ya Nzega mjini Magharibi. Mama huyu kabla ya kujiunga na TASAF aliishi katika nyumba yenye kuta za maturubai ambapo hakuwa na chanzo cha uhakika cha kujiingizia kipato wala hakuweza kupata milo mitatu kwa siku. Baada ya kusajiliwa TASAF kwa sasa ameweza kuanza kujenga nyumba na kununua mbuzi na kuwafuga kwa kuwekeza kidogo kidogo. “nilianza kupokea ruzuku mwaka 2015 malipo yangu ya kwanza na ya pili niliyatumia kwa mahitaji ya nyumbani,walipaji kutoka TASAF walikua wakitoa elimu kuhusu umuhimu wa kuweka akiba kidogo kidogo ndipo nilipoamua kufanya hivyo na hivi sasa najionea matunda” alisema Consolata
Naye Simion Ntemanya(50) Baba wa watoto wanne anayeishi na familia ya watu sita ambaye kupitia mpango huu ameweza kuanzisha biashara ya magodoro ya pamba anasema “nilianza kutengezeza godoro moja na kuliuza sh. 6000 hadi sh.7000 na kupata faida ya Sh.3000 hadi 4000 kwa godoro moja, sasa naweza kutengeneza magodoro manne kwa mwezi hivyo faida imeongezeka.shughuli hii naifanya wakati wa kiangazi msimu wa kilimo siwezi kuifanya kwani nakuwa shambani kwa ajili ya kilimo”
Akizungumza, Bi. Rejina kulwa (50),mkazi wa kijiji cha kitangiri ambaye ni mama watoto sita mnufaika wa mpango wa TASAF yeye aliweza kununua kuku watano hadi kufikisha kuku 40 “Kuku walipofika 40 niliwauza na kununua mbuzi wawili jike ambao hadi kufikia mwaka 2018 nilikua na mbuzi 30 nikawauza mbuzi wote na kununua ardhi”alisema Bi.Rejina
Baada ya kununua ardhi aliweza kupanda mbegu ya mpunga na kuvuna magunia 30 na kuyauza alipata kiasi cha sh.1,600,000/=. Bi.Rejina aliamua kununua ng’ombe wadogo saba na kuwafuga kwa muda wa mwaka mmoja na baadaye mwaka 2019 aliwauza ng’ombe wanne na kununua ng’ombe mmoja mwenye nguvu ili kupata ngombe wa kulimia shamba.
Bi.Rejina ameendelea kufanya shughuli za kilimo na kufanikiwa kujenga nyumba yake ambapo sasa anaishi na watoto wake sita.
Bw. Denis Kazinja anawashauri Walengwa kuendelea kuwekeza katika shughuli mbalimbali za uzalishaji mali kwa kutumia ruzuku wanazoendelea kupata ili ifikapo mwisho wa mradi huu wawe wamekwisha kuwa na uwezo wa kujitegemea.
NZEGA TOWN COUNCIL (HALMASHAURI YA MJI NZEGA)
Sanduku la Barua: S.L.P 256 NZEGA-TABORA
Simu ya Mezani: +255677003373
Simu ya Mkononi: +255677003373
Barua Pepe: td@nzegatc.go.tz
Haki miliki zote zimehifadhiwa na nzegatc 2017