Na James Kamala, Afisa Habari
Mchakato wa kujiandikisha, kampeni, kuwasilisha sera za wagombea, na kupiga kura umehitimishwa kwa mafanikio na amani katika Halmashauri ya Mji wa Nzega. Viongozi wa maeneo mbalimbali wameonyesha umahiri wao, huku uchaguzi huo ukiwa nguzo mshikamano na ushiriki wa wananchi kwenye kutekeleza haki yao ya msingi.
Msimamizi wa Uchaguzi, ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Nzega, Bw. Shomary Salim Mndolwa, aliwasihi wasimamizi wa vituo vya kupigia kura kuhakikisha haki inatendeka na kushirikiana kikamilifu na wananchi.
"Hakikisheni mnatoa haki sawa kwa wapiga kura wote ili waweze kushiriki kikamilifu. Kuweni waaminifu na simamieni zoezi hili kwa kumtanguliza Mungu ili mpate nguvu na utulivu na umahiri katika kazi yenu," alisema Bw. Mndolwa.
Mafunzo waliyopatiwa wasimamizi yalisaidia kufanikisha zoezi hilo kwa weledi, kwani hadi zoezi linakamilika hakukuwa na ripoti zozote za ukiukwaji wa maadili. Mchakato mzima uliendeshwa kwa amani, na matokeo yalifanikisha lengo la maendeleo endelevu ya Halmashauri ya Mji wa Nzega na Taifa kwa ujumla.
Waziri wa Kilimo na Mbunge wa Jimbo la Nzega Mjini, Mhe. Hussein Bashe, aliungana na wakazi wa Mtaa wa Humbi, Kata ya Nzega Mjini Magharibi, kushiriki katika zoezi hilo. Baada ya kupiga kura, Mhe. Bashe aliwashukuru wananchi kwa kujitokeza kwa wingi na kushiriki kikamilifu katika kutimiza haki yao ya kikatiba.
"Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa ufanisi wa zoezi hili. Hakuna jambo kubwa lililoathiri demokrasia yetu. Nawapongeza wananchi na wagombea wote, hasa wale wa Chama Cha Mapinduzi, kwa kuendesha kampeni za heshima na amani," alisema Mhe. Bashe.
Vijana wa kike na wa kiume walijitokeza kwa wingi na kueleza kuridhika kwao na maandalizi mazuri ya uchaguzi, ambao ulifanyika haraka na kwa ufanisi, bila kuathiri ratiba zao za kila siku.
Uchaguzi huo pia ulisimamiwa na mawakala wa vyama vya siasa walioteuliwa rasmi kuwakilisha vyama vyao kwenye vituo vya kupigia kura. Ushirikiano huu ulidhihirisha umuhimu wa maadili na uwazi katika kuimarisha demokrasia.
NZEGA TOWN COUNCIL (HALMASHAURI YA MJI NZEGA)
Sanduku la Barua: S.L.P 256 NZEGA-TABORA
Simu ya Mezani: +255677003373
Simu ya Mkononi: +255677003373
Barua Pepe: td@nzegatc.go.tz
Haki miliki zote zimehifadhiwa na nzegatc 2017