Jumla ya watoto 16,442 wenye chini ya umri wa miaka mitano wanatarajiwa kupata chanjo ya kuwakinga dhidi ya maambukizi ya magonjwa ya Surua na Rubella katika Halmashauri ya Mij wa Nzega.
Hayo yamebainishwa na Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji wa Nzega, Dkt Anna Godwin Chaduo wakati wa uzinduzi wa Zoezi hilo litakalochukua takribani siku nne kufikia idadi tajwa hapo.
“Wazazi na walezi wanasisitizwa kupeleka watoto kwenye vituo vya chanjo vilivyotengwa ili kuhakikisha wanapatiwa chanjo ya kuwakinga na magonjwa ya mlipuko,” alisema Dkt Chaduo na kuongeza kuwa chanjo hizi ni salama na zimegharimiwa na serikali ili kulinda afya ya watoto ambao ni taifa la kesho.
Alisisitiza kuwa tayari baadhi ya nchi jirani zimepata milipuko ya magonjwa hayo na mengine ambayo yameathiri watoto na watu wazima, na hivyo ni muhimu sana kwa wazazi wilayani NZega kuchukua tahadhari kwa kuhakikisha kila mtoto anapata chanjo hiyo bila kukosa.
Alifafanua kuwa kwa watoto waliowahi kupata chanjo huko nyuma, ni muhimu wapate chanjo ya nyongeza (booster shot) ili waweze kuwa salama kwa kupata kinga kwa asilimia mia moja.
Kwa upande wake, Mratibu wa Chanjo wa Halmashauri ya Mji wa Nzega Bw. Mohamed Kitivo, alisema kuwa vimeandaliwa vitua 13 vya kuendesha zoezi hilo na kwamba wazazi na walezi wafikena watoto wao bila kukosa katika ya saa mbili asubuhi hadi saa kumi namoja jioni.
Bw. Kitivo alifafanua ya Kuwa, vituo vilivyoandaliwa kutoa chanjo ni pamoa na Vituo vya afya viwili, Zahanati kumi, pamoja na hospital ya Mji Nzega. Pia, vimeandaliwa vituo vya muda kwa maeneo yaliyoko pembezoni kama vile ofisi za serikali, shule nakadhalika ili kupunguza usumbufu wa kusafiri kwenda mbali kutafuta huduma hiyo ya chanjo
“Zoezi hili litachukua siku nne mpaka tano na tumejipanga kuhakikisha linafanikiwa kwa asilimia mia moja ili kuhakikisha hakuna mtoto anayeachwa bila kuchanjwa na kupata kinga inayohitajika,” Alisema.
Mgeni rasmi katika uzinduzi wa zoezi hili alikuwa ni Mkuu wa Wilaya ya Nzega Mhe. Naitapwaki Tukai aliyewakilishwa na Afisa Tawala wa Wilaya ya Nzega Bi. Amina Suleiman Matua.
NZEGA TOWN COUNCIL (HALMASHAURI YA MJI NZEGA)
Sanduku la Barua: S.L.P 256 NZEGA-TABORA
Simu ya Mezani: +255677003373
Simu ya Mkononi: +255677003373
Barua Pepe: td@nzegatc.go.tz
Haki miliki zote zimehifadhiwa na nzegatc 2017