Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Dorothy Gwajima, amepongeza hatua za kukamatwa kwa watumishi watatu wa Zahanati ya Miguwa ilioyoko Nzega Mjini kwa tuhuma za kuhusika katika kifo cha mwanafunzi kwenye jaribio la utoaji mimba.
Waziri Dkt. Gwajima alitoa pongezi hizo Mjini Nzega, Mkoa wa Tabora Jumanne ya tarehe 23/10/2024 wakati wa zoezi la kuweka jiwe la msingi kwenye Ujenzi wa barabara na daraja kubwa katika kata ya Ijanija Mjini Nzega, linalolenga kuimarisha upatikanaji wa huduma za jamii kwa wakazi wa maeneo hayo.
“Nampongeza Mkuu wa Mkoa Tabora kwa kuwezesha kukamatwa kwa watumishi wa Kituo cha Afya Miguwa pamoja na wazazi wanaotuhumiwa kuhusika na kifo cha mtoto huyo,” Dkt. Gwajima alisema na kuongeza kwamba juhudi za kupambana na ukatili dhidi ya watoto zinakwama pale matendo hayo yanapofanywa na ndugu wa karibu, ikiwemo wazazi.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mhe. Paul Matiko Chacha, alimueleza Waziri Dkt. Gwajima kuwa binti mmoja mkazi wa kijiji cha Miguwa aliyehitimu elimu ya shule ya msingi mwaka huu alihisiwa kuwa na uhusiano wa kimapenzi na babake mzazi. Mhe. Matiko alieleza kuwa mama wa kambo wa binti huyo aligundua hilo na kumuonya mumewe, lakini hakuchukua hatua za kutosha kuachana na matendo hayo.
“Kitendo hicho haramu kilendelea hadi pale ilipobainika kuwa binti alikuwa na ujauzito wa baba yake. Walijaribu kutoa ujauzito huo kwa usaidizi wa mkuu wa Zahanati ya Miguwa. Zoezi hili lilifanyika usiku, na binti alipata maumivu makali ambayo yalisababisha kifo chake,” alisema Mhe. Matiko.
Aidha, baada ya kifo chake, juhudi za kificho zilifanyika ili kuuzika mwili wa binti huyo katika kijiji kingine, lakini vyombo vya ulinzi na usalama Wilayani Nzega viliingilia kati na kuwakamata wazazi hao pamoja na wahudumu wa afya wanaotuhumiwa. Uchunguzi unaendelea na wahusika watafikishwa mahakamani.
Imeadaliwa na James Kamala, Afisa Habari – Nzega Mji.
NZEGA TOWN COUNCIL (HALMASHAURI YA MJI NZEGA)
Sanduku la Barua: S.L.P 256 NZEGA-TABORA
Simu ya Mezani: +255677003373
Simu ya Mkononi: +255677003373
Barua Pepe: td@nzegatc.go.tz
Haki miliki zote zimehifadhiwa na nzegatc 2017