KAMATI YA USHAURI YA HALMASHAURI YA MJI WA NZEGA YAPITISHA RASIMU YA BAJETI YA SHILINGI BILIONI 26.
Kamati ya Ushauri ya Baraza la Halmashauri ya Mji wa Nzega imejadili na kupitisha rasimu ya bajeti yenye jumla ya Shilingi Bilioni 26 kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Kikao hicho kilifanyika chini ya Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Nzega, Mhe. Naitapwaki Tukai, ambapo jumla ya Shilingi 26,159,230,860 zilipitishwa kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo na uendeshaji wa halmashauri kwa mwaka wa fedha ujao.
Akisoma taarifa ya rasimu ya bajeti hiyo mbele ya Baraza, Mkuu wa Idara ya Mipango wa Halmashauri ya Mji wa Nzega, Bi. Joyce Emanuel, alieleza kuwa zaidi ya asilimia 16 ya bajeti hiyo, sawa na Shilingi 4,391,509,900, inatarajiwa kukusanywa kutoka kwenye vyanzo vya mapato ya ndani ya halmashauri. Aidha, Shilingi 21,767,720,960 zinatarajiwa kupatikana kupitia ruzuku kutoka Serikali Kuu.
Kikao hicho kilihudhuriwa na Wakuu wa Idara na Vitengo mbalimbali vya Halmashauri ya Mji wa Nzega, Waheshimiwa Madiwani, viongozi wa vyama vya siasa, pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Nzega.
Akizungumza katika kikao hicho, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Nzega, Mhe. Paskali Kigalu, aliishukuru Kamati ya Ushauri kwa kupokea na kupitisha rasimu ya bajeti hiyo, akisisitiza kuwa wataalamu wa halmashauri wako tayari kufanya kazi kwa bidii na weledi ili kuhakikisha bajeti hiyo inatekelezwa ipasavyo.
“Tunashukuru sana kamati hii kwa kupokea na kupitisha rasimu hii ya bajeti. Wataalamu wako tayari kuchapa kazi kwa moyo na kwa weledi ili kuhakikisha inatekelezwa kwa ufanisi mkubwa,” alisema Mhe. Kigalu.
Mhe. Kigalu pia alitoa wito kwa wadau wote wa Baraza la Ushauri kushirikiana kwa karibu na wataalamu wa Halmashauri ya Mji wa Nzega ili kuhakikisha bajeti hiyo inatekelezwa kwa mafanikio na kuleta maendeleo endelevu kwa wakazi wa Nzega na Taifa kwa ujumla
NZEGA TOWN COUNCIL (HALMASHAURI YA MJI NZEGA)
Sanduku la Barua: S.L.P 256 NZEGA-TABORA
Simu ya Mezani: +255677003373
Simu ya Mkononi: +255677003373
Barua Pepe: td@nzegatc.go.tz
Haki miliki zote zimehifadhiwa na nzegatc 2017