Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Nzega afariki kwa ajali
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Nzega, Mhe. Paschal Kigalu, amefariki dunia katika ajali ya barabarani iliyohusisha magari mawili kugongana uso kwa uso.
Ajali hiyo ilitokea alfajiri ya tarehe 18 Februari 2026 katika eneo la Kitangili, ikihusisha gari aina ya Range Rover Vogue na Toyota Kluger, mali ya mwenyekiti huyo.
Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mji wa Nzega, Dkt. Sephania Muyanga, amethibitisha kupokea miili miwili ya marehemu waliofariki kufuatia ajali hiyo.
“Tumepokea miili miwili ya wanaume waliofariki kwenye ajali hiyo, ukiwemo wa Bwana Kigalu na mwingine ambaye bado hajafahamika. Pia tumepokea majeruhi kadhaa ambao idadi yao itajulikana baadaye, na taratibu za kunusuru maisha yao zinaendelea,” alisema Dkt. Muyanga.
Mhe. Kigalu amefariki dunia ikiwa ni miezi miwili tu tangu achaguliwe na Baraza la Madiwani kuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Nzega. Aliibuka mshindi katika uchaguzi wa baraza hilo uliofanyika tarehe 5 Desemba 2025, kufuatia ushindi wake wa kiti cha udiwani wa Kata ya Itilo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi wa tarehe 29 Desemba 2025.
Mbunge wa Jimbo la Nzega Mjini, Mhe. Hussein Bashe, amesema kuwa marehemu ameacha pengo kubwa, na amewaomba wananchi kumuombea apumzike kwa amani.
“Tumepatwa na msiba mzito. Taratibu za mazishi zitatangazwa baadaye. Tuendelee kumuombea pumziko la milele,” alisema Mhe. Bashe wakati akifungua hafla ya kupongeza walimu kwa ufaulu bora wa shule za Mji wa Nzega
NZEGA TOWN COUNCIL (HALMASHAURI YA MJI NZEGA)
Sanduku la Barua: S.L.P 256 NZEGA-TABORA
Simu ya Mezani: +255677003373
Simu ya Mkononi: +255677003373
Barua Pepe: td@nzegatc.go.tz
Haki miliki zote zimehifadhiwa na nzegatc 2017