Ikiwa ni siku chache baada ya Makamu wa Rais, Dkt. Philip Isdor Mpango, kuwataka wakazi wa Halmashauri ya Mji wa Nzega na Watanzania kwa ujumla kujitokeza kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura na baadaye kupiga kura, tayari wito huo umeendelezwa na viongozi wengine wa ngazi ya jamii.
“Nawataka bodaboda wenzangu, familia zao na wananchi kwa ujumla kutumia muda uliotolewa kujiandikisha na kupiga kura kwenye daftari maalum kwa muda uliopangwa. Hii ni haki ya kikatiba ya kuchagua viongozi tunaowataka,” alisema Yohana Bujilima, Mwenyekiti wa Kikundi cha Waendesha Bodaboda eneo la Ushirika Mjini Nzega.
Bujilima aliendelea kuwaasa bodaboda wenzake na vijana kwa ujumla kufika kwenye vituo vya kujiandikisha wakiwa watulivu na kufuata utaratibu uliowekwa na wasimamizi wa zoezi hilo bila kusababisha vurugu.
Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Humbi, ulioko Kata ya Nzega Mjini Magharibi, Bw. Charles Makala, aliwahamasisha wakazi wa mtaa wake kuwa kujiandikisha na kupiga kura ni jambo muhimu sana na wasikose kutumia vizuri nafasi hiyo ya kushiriki kwenye uchaguzi.
“Tujitokeze kwa wingi maana tunahitaji kuchagua viongozi wa serikali za mtaa wanaotufaa. Tuitumie nafasi hiyo vizuri sana kwa faida yetu wenyewe,” alisema.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji wa Mtaa wa Ipilili, Bi Elizabeth Msengi, alisema ofisi ziko wazi kwa siku kumi na moja zilizotengwa kwa ajili ya zoezi hilo. Akiongea na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini mtaani Ipilili, Bi Msengi alisema ofisi ziko wazi, hivyo wananchi wasisite kujitokeza kwa wingi.
Zoezi la kuandikisha wapiga kura litaendeshwa kuanzia tarehe 11 hadi 20 Oktoba mwaka huu, huku zoezi la kupiga kura likitarajiwa kufanyika tarehe 27 Novemba. Katika zoezi hilo, wananchi wa Nzega na Watanzania kwa ujumla watachagua wenyeviti na wajumbe wa vijiji, mitaa, na vitongoji.
Imeandaliwa na James Kamala, Afisa Habari – Nzega Mji.
NZEGA TOWN COUNCIL (HALMASHAURI YA MJI NZEGA)
Sanduku la Barua: S.L.P 256 NZEGA-TABORA
Simu ya Mezani: +255677003373
Simu ya Mkononi: +255677003373
Barua Pepe: td@nzegatc.go.tz
Haki miliki zote zimehifadhiwa na nzegatc 2017